Ujio wa Lwandamina umewaweka mguu ndani mguu nje Chirwa na Twite kwani anataka kusajili wachezaji wapya na kukata majina ya wawili hao Jangwani
Baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kocha mpya wa Yanga Mazambia George Lwandamina ameanza kukifumua kikosi hicho baada ya kupendekeza jina la mshambuliaji wa kimataifa wa Kenya Jesse Were asajiliwe kipindi hiki cha dirisha dogo.
Katibu mkuu wa Yanga Baraka Desidedit, ameiambia Goal , Lwandamina anataka kusajili nyota wawili wapya kutoka klabu ya Zesco aliyokuwa akiifundisha kabla ya kutua Yanga mmoja wapo akiwa Were anayecheza nafasi ya ushambuliaji na kiungo mkabaji Meshack Chaila ambaye jina lake ndiyo lilikuwa la kwanza kupendezwa na kocha huyo.

“Kocha ametoa mapendekezo yake ya wachezaji anaotaka kuwasajili kipindi hiki cha dirisha dogo, ambao ni Were na Chaila sasa hapo niwazi Mbuyu Twite na Chirwa wanaweza kukatwa ili kutoa nafasi ya wachezaji hao wawili kusajiliwa na majina hayo ya wachezaji wa kutemwa ameyapendekeza yeye,” amesema Baraka.
Katibu huyo amesema kama uongozi wameshaanza kuyafanyia kazi mapendekezo ya kocha huyo na watahakikisha wanazinasa saini za wachezaji hao ili kumrahisishia kazi kocha wao.
Amesema Lwandamina amevutiwa kwa kiasi kikubwa na kikosi cha Yanga, na ameahidi kuipa ubingwa katika msimu wake wa kwanza endapo ataongezewa nguvu kwa kuwapata wachezaji hao wawili aliowapendekeza.
“Sizani kama kuna kitakachoshindana kwasababu tumeshazungumza na wachezaji hao wote pamoja na uongozi wa timu yao kila kitu kinakwenda vizuri na wachezaji hao wanatarajiwa kuwasili muda wowote kwa ajili ya kusaini mikataba ili waweze kuwa mali yao,”amesema Baraka.
Lwandamina anatarajiwa kuanza kazi Novemba 25, hiyo ikiwa ni baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuifundisha Yanga,akichukua nafasi ya Mdachi Hans van der Pluijm aliyeifundisha timu hiyo kwa mafanikio makubwa katika misimu miwili na kuipa ubingwa wa ligi ya Vodacom mara mbili mfululizo.