Mzunguko wa pili Yanga haitakuwa na Hans van der Pluijm kama kocha wao, lakini kocha huyo hajuti kulingana na rekodi nzuri aliyo nayo Jangwani
Pluijm ameiambia Goal, bado hajajua hatima yake ndani ya klabu hiyo, lakini kitendo cha kubeba taji mara mbili na kumaliza mzunguko wa kwanza kwenye nafasi ya pili msimu huu vinamfanya kujivuna kwa kazi nzuri aliyoifanya ingawa wapo baadhi ya watu hawalioni hilo.
“Naweza nisiwe kocha wa Yanga kwenye mzunguko wa pili lakini najivuni mwenendo mzuri wa timu yangu hadi kumaliza mzunguko wa kwanza nafasi ya pili hii ni ishara kwamba tunao uwezo wa kuwa tena mabingwa kwa mara ya tatu,”.
“Lakini siyo hilo tu pia rekodi yangu ndani ya Yanga ni nzuri kiasi cha kunipa matumaini kwamba siwezi kukosa timu ya kufundisha kutokana uzoefu na uwezo wa kufundisha soka Barani Afrika,” amesema Pluijm.
Mdachi huyo pia amezungumzia ushindani aliokutana nao kwenye mzunguko wa kwanza msimu huu na kusema umekuwa mkubwa tofauti na misimu iliyopita.
Pluijm amesema timu nyingi msimu huu hata zile ngeni zinazoshiriki kwa mara ya kwanza ligi zimeonyesha ushindani wa hali ya juu na kuzipa wakati mgumu timu kubwa.
“Tulicheza na Mbao hadi mapumziko tulikuwa hatuja wafunga, licha ya kuwatumia nyota wetu wote lakini hata kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Ruvu Shooting ilitulazimu kutumia uzoefu na uwezo binafsi wa nahodha wetu Haruna Niyonzima ndiyo kupata pointi tatu,” amesema Pluijm
Kuna uwezekano mkubwa Yanga wakamwondoa Pluijm na nafasi yake kuchukuliwa na kocha Mazambia George Lwandamina ambaye tayari yupo Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo na kusaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo kuanzia mzunguko wa pili unaotarajia kuanza Januari 2017.


0 comments:
Post a Comment